MKUU WA IDARA AHITIMISHA SEMINA YA WANAWAKE NA WATOTO DORCAS

Mkuu wa Idara ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii Mchg. Peweni Kikoti ameongoza Ibada ya Siku ya Bwana ya 13 baada ya Utatu na kuhitimisha Semina ya Wanawake wa Usharika wa Mazoezi Galilaya Nsumba iliyofanyika kwa siku 8 kuanzia tarehe 23 - 30.08.2026 ikiwa ni hitimisho la maadhimisho ya Ibada ya Mwezi Agosti ambayo hufanyika kila mwaka kidayosisi (DMZV) kwa ajili kukumbuka kuanzishwa Kitengo cha Wanawake na Watoto - Dorcas. Katika Ibada hiyo Mchg.Peweni Kikoti amewakumbusha wakristo kuishi maisha ya Unyenyekevu katika familia, Kanisa na Jamii ili Mungu aweze kuachilia baraka zake. Aliendelea kusema kuwa mtu hawezi kuwa mnyenyekevu ikiwa anaishi na uchungu au maumivu moyoni mwake dawa pekee katika kuondoa uchungu moyoni ni kusamehe. Wakristo wanatakiwa kuitafuta furaha, amani na Upendo ili kudumisha umoja na mshikamano na kuepuka migogoro. Aidha wazazi wana wajibu wa kuishi kwa mfano ili watoto wao wajifunze mema kutoka kwao.