ETE KUENEA KKKT, DAYOSISI ZA ZIWA VICTORIA NA MAGHARIBI. Semina ya Elimu ya Theologia kwa Enezi (ETE) iliyoendeshwa tarehe 11 na 12 Novemba 2026 Jijini Mwanza katika Kituo cha Mikutano Charming Bungalow Nyakato, imezaa wazo la kuwa na Ushirikiano utakaowezesha ETE kuenea katika kanda hii. Awali, mfumo wa kujisomea Theologia kwa madarasa pasipo kujiunga Vyuoni (ETE) ulikuwa ukiendeshwa katika Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria - DMZV tu na baadaye Dayosisi ya Magharibi Kati. Semina hii imeendeshwa na Mchg Stefano kutoka Swedish Evangelical Mission (SEM) na Wachungaji waratibu wa ETE, Elia Konga na Milton Mbosa kutoka Dayosisi ya Iringa ikilenga kuongeza kasi ya ukuaji wa ETE kwa kutumia mtandao (TEE Online) Wajumbe waliohudhuria ni Wasaidizi wa Maaskofu na Wachungaji/Waratibu kutoka Dayosisi za; Mashariki ya Ziwa Victoria, Mkoani Mara, Magharibi Kati - Tabora, Magharibi - Kigoma na Karagwe. Katika Semina hii, Mchg Daniel Machibya wa KKKT-DMZV alichaguliwa kuwa Mratibu wa ETE wa ukanda huu.